Sifa Kumi Zitakazo kufanya kuwa mjasiriamali shupavu

Nataka utambue kuwa zipo sifa zaidi ya 10 ya zile nitakazokutajia hapa; kwani naamini hata wewe unaweza ukawa na sifa unayoiona kwako imekufanya uwe mjasiriamali uliyefanikiwa na kupata kibali kwa watu dhidi ya biashara yako.

Ila ni vyema katika hilo nami nikukumbushe sifa 10 muhimu ambazo ndio msingi muhimu zidi ya kila mjasiriamali yoyote yule duniani anayehitaji kufanikiwa; unahitaji kuzijua sifa hizi kama wewe ni mjasiriamali au si mjasiriamali kwa wakati huu ila ni kwa hapo badae zitakuwa na faida kwako.
Kwa kufahamu sifa hizi 10 za mjasiriamali wa kweli itakupa kujipima kiupande wako kama kweli sifa hizi unazo maishani mwako au hauna ila unahitaji kuzifahamu na kuzitumia.
Kwa maelezo mafupi lakini yenye tija na utoshelevu wa kiwango cha juu kwako; nimejaribu kukuelewesha juu ya kila sifa japo hata kwa ufupi ili uweze kuelewa sifa hizi kiundani zaidi.
Hebu tuangalie sifa hizo kwa undani kidogo; hata kwako wewe ambaye si mjasiriamali hebu soma hapa ili uweze kupata ufahamu utakaokusaidia hapo badae.
Kumbuka tu kwamba dunia ya sasa tuliyonayo ni dunia ya ujasiriamali na biashara. Asilimia 90% ya mamilionea na bilionea ni watu wenye kujishughulisha na suala zima la ujasiariamali au kwa lugha nyepesi wanamiliki biashara zao binafsi.
Sifa ya Kwanza:
Ni Mwenye Imani.
Kwa lugha nyepesi mjasiriamali ni mtu mwenye uhakika na kile anachotaka kufanya au anachofanya; hana hofu na mashaka juu ya anachotaka kufanya au kuwekeza.
Hana hofu juu ya biashara anayoiendesha; na sababu hiyo yupo tayari kwa lolote lile litakaloweza kutokea katika biashara yake aliyonayo au aliyoianzisha.
Sifa ya Pili:
Moyo wa Udhubutu.
Ni mwenye kujaribu kile anachoona anaweza kufanya na kinachoweza kumletea faida halisi katika maisha yake binafsi na ya biashara yake. Hana mashaka na yupo tayari kujaribu kila fursa inayojitokeza mbele yake.
Mjasiriamali si mtu mwenye hofu ya kujaribu kuingia katika fursa mpya inayojitokeza mbele yake. Ilimradi ana uwezo na udhibitisho wa kutosha unaomruhusu kuingia na kutekeleza wazo lake zuri alilonalo la biashara.
Sifa ya Tatu:
Mbunifu.
Hii ni mojawapo ya maana kamili na halisi ya mjasiriamali kama ulikuwa hufahamu. Kama hakuna ubunifu basi hakuna mjasiriamali; na hakuna mjasiriamali nje ya ubunifu. Hivyo mjasiriamali ni mbunifu.
Huwezi kuwa mjasiriamali wa kweli hadi umebuni; na hasa umebuni kile unachotaka kutoa au kufanya katika soko kwa mara ya kwanza. Mjasiriamali ni yule anayeona mambo mapya kila siku na kuyaleta katika uhalisia wake.
Sifa ya Nne:
Mwenye Maono.
Mjasiriamali ni mtu anayeona mbele zaidi ya wengine waliomzunguka; anayeona mbali zaidi ya wengine; anayeona mambo kwa hali chanya na si hasi. Huwezi kufikia kuwa Mjasiriamali kama hujioni kuwa mjasiriamali.
Utakuwa Mjasiriamali wa kweli ni baada ya kujiona wewe ni mjasiriamali kupitia akili na moyo wako hasa katika kile ulichoanza kufanya. Na baada ya kuwa mjasiriamali halisi unaanza kuona zaidi ya hapo kwanza ulivyoona kabla ya kuwa mjasiriamali.
Sifa ya Tano:
Anafanya Kazi kwa Bidii na Ujuzi.
Ndio maana ya pili ya mjasiriamali. Ni kufanya kazi kwa juhudi na bidii kwa kupitia ujuzi alionao ili kufikia maono na malengo makubwa aliyonayo kabla ya kuwa mjasiriamali halisi.
Kufanya kazi kwa bidii ndio kunamsukuma mjasiriamali kufikia katika maono na malengo yake aliyokuawa amejiwekea kuyafikia; na zaidi ya yote ni kufanya kazi kwa bidii chini ya ujuzi wake alionao ndani yake.
Sifa ya Sita:
Yupo huru na Anachofanya.
Hana hofu na alichokichagua kukifanya. Bali yupo huru na anachofanya usiku na mchana ilimradi afikie malengo na maono yake makubwa aliyonayo moyoni.
Lakini zaidi ya hilo anakuwa huru na kazi yake yeye mwenyewe anayoifanya; hii ni tofauti sana na wale walioajiriwa katika taasisi mbali mbali ziwe taasisi binafsi au za kiserikali.
Yupo huru kujipangia muda wake wa kazi, yaani muda wake wa kufungua na kufunga biashara yake; kununua na kuuza bidhaa au huduma yake, kuchagua soko la bidhaa zake, kuchagua aina ya wateja awatakao nk.
Sifa ya Saba:
Ni Mwenye Malengo Mapya.
Mjasiriamali ni mtu mwenye malengo mapya kila siku. Hauwezi kuwa mjasiriamali unayetembea na wazo lile lile moja uliloanza nalo mwanzoni mwa biashara yako; pasipo kuongeza wigo wa upana wa malengo yako sawa na mabadiliko ya dunia inavyokwenda.
Hivyo basi mjasiriamali ni mtu mwenye malengo mapya; lakini si tu kuwa na malengo mapya bali anajua ni namna gani ya kuyasimamia malengo hayo na kuyawekea mpangomkakati wa kuyatimiza.
Sifa ya Nane:
Hakati Tamaa.
Na hii ndio sifa inayowafanya wajasiriamali wengi wawe tofauti, yaani watofautiane na wengine. Suala la kutokukata tamaa ni suala la muhimu sana kwa mjasiriamali yoyote yule anayehitaji kufikia mafanikio makubwa katika kile alichokianzisha.
Hata kama umefanya makosa mara kadhaa, umedharauliwa, umepata hasara, umepata matatizo ya kifedha au familia nk. Lakini si vyema ukate tamaa haraka bali ni vizuri uzidi kubaki ukitazama kwenye ndoto yako uliyonayo ili kuitimiza au kufanikisha kile ulichokianza.
Sifa ya Tisa:
Anakubali Mabadiliko.
Hauwezi kuwa mjasiriamali wa kweli katika dunia hii ya leo kama hautokubaliana na mabadiliko yoyote yale yanayojitokeza duniani. Kukubaliana au kwenda na mabadiliko ni uamuzi wako wewe binafsi.
Mabadiliko kama vile ya masoko, bei kupanda na kushuka, teknolojia, sheria zilizokuzunguka, uchumi wa eneo ulipo, mazingira ya kibiashara, kushuka kwa shilingi, gharama za kulipa kodi au ushuru, nk. Ni vizuri mabadiliko kama hayo ukubaliane nayo na uwe tayari kupambana nayo katika hali yoyote ile, ili uweze kutimiza ndoto zako na si kukata tamaa.
Sifa ya Kumi:
Mtafutaji wa Maarifa.
Hii ndio sifa inayotimiza sifa kumi za mjasiriamali wa kweli kutoka katika mtandao huu wa Ishi Ndoto Yako. Ni vyema utambue unapaswa kuwa na msingi mzuri zaidi wa kujisomea ili kutafuta maarifa mapya kila siku kwa ajili ya kuboresha biashara yako uliyoamua kuwekeza.
Biashara yako haiwezi kuendana na ushindani uliopo katika soko la dunia ya leo; kama hautoweza kuwa mtu wa kutafuta taarifa mpya kila leo hasa kwa kutafuta maarifa mapya kila siku iitwapo leo.
Tembelea mtandao huu wa Ishi Ndoto Yako na mitandao mingine yenye kutoa mafunzo kuhusu ujasiriamali na biashara kila siku; ili uweze kujipatia maarifa na ujuzi wa kutosha wa kukusaidia katika kuboresha na kuendeleza biashara yako.
Hadi kufikia hapo nakutakia mafanikio mema katika maisha yako na zaidi uwe mjasiriamali wa kweli kwa ajili ya kulijenga taifa lako na dunia kiujumla.

Artikel Terkait