Hiki ni kizimba bora ambacho kinaonyesha kwamba juu kuna kizimba cha kuishi na chini ni kwa ajili ya sungura kucheza.
Na Daniel Mbega
MPENDWA mjasiriamali,
utakumbuka kwamba katika mfululizo wa makala hizi za ufugaji wa sungurakibiashara tumejifunza mambo
mbalimbali ikiwemo uanzishwaji wa biashara hiyo ya mifugo, faida zitokanazo na ufugaji huo pamoja na aina mbalimbali zasungura wanaofaa kufugwa kwa matumizi mbalimbali.
Katika makala haya,
tunaangalia namna ya ujenzi wa mabanda bora ya sungura ili wakuletee faida
katika kipindi ambacho kuna mahitaji makubwa ya nyama.
Huku tukiangazia Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya 2025 ambayo inataka Watanzania wawe katika uchumi wa
kati, pamoja na kuzingatia Maendeleo Endelevu ya Dunia yanayotaka kukomeshwa
kwa umaskini pamoja na kuongeza upatikanaji wa chakula, biashara ya ufugaji wa
sungura ni muhimu kuizingatia.
Najua faida ya mifugo
kwa sababu nimezaliwa na kukulia katika mazingira ya ufugaji ingawa wakati huo
hakukuwa na maendeleo kama ya sasa.
Leo hii ninapozungumzia
fugaji wa sungura natambua kwamba uwekezaji huo unaweza kukuletea tija katika
njia nyingi tu kama kuuza mkojo wa sungura kwenye maabara mbalimbali, kupata
samadi kutokana na kinyesi chao ambacho pia hutumika kuzalishia mionyoo. Nyama,
hata hivyo, ndiyo bidhaa kubwa na muhimu.
Ninachotaka kuwaelekeza
hapa wajasiriamali wenzangu ni kitu rahisi tu katika uanzishaji wa ufugaji wa
sungura kwa kuanzia na kile ulichonacho, siyo kama wanavyoelekeza wale
wanaoitwa wataalamu.
Tunafahamu hali zetu za
uchumi zilivyo, hivyo tukianza kuwaza kuhusu mtaji mkubwa kamwe hatuwezi
kufanikiwa kwenye ujasiriamali.
Kwa maana hiyo,
tunapaswa kuanza katika mazingira tuliyopo, kwa rasilimali zilizopo na tunaweza
kukua taratibu hadi kufikia kwenye uwekezaji mkubwa katika ufugaji wa sungura.
Nitajaribu kueleza hatua
kwa hatua tangu unapoanza ufugaji kwa mara ya kwanza na kueleza ni kwa vipi
unaweza kukabiliana na changamoto ambazo hazijaandikwa kwenye vitabu au
miongozo mingine. Lakini daima kumbuka kwamba, uzoefu ni mwalimu mzuri katika
ujasiriamali.
Mambo ya msingi
Kuna mambo
mengi ambayo unapaswa kuyafahamu kabla ya kuanza ufugaji wa sungura. Lakini
nitajaribu kueleza kwa nia ya kukupa mwangaza wa namna ya kuanzisha ufugaji
huo.
Kadiri
unavyoendelea, na ikiwezekana, unatakiwa kupata taarifa za kutosha kuhusu
ufugaji huo, kuanzia ujenzi wa mabanda, jinsi ya kuwahudumia, uchunaji wake
baada ya kuwachinja, kuweka kumbukumbu na kadhalika.
Binafsi naweza
kutumia dakika tano tu kumchuna sungura, tofauti na unavyotumia muda mrefu
kunyonyoa kuku.
Sungura hawana
msimu wa kuwafuga, unaweza kuanza ufugaji wakati wowote na wanaweza kuanza kuzaliana
wakati wowote, tofauti na wanyama wengine.
Sungura majike
wawili na dume moja wanaweza kukupatia wewe na familia yako kiasi cha kilogramu
81 za nyama kwa mwaka, kiasi ambacho ni kingi kwa familia za wastani wa watu
watano.
Ujenzi wa Banda
Kumbuka: vizimba hivi ni
sawa na vile vinavyotumiwa katika ufugaji wa kuku ingawa hivi vya sungura
vinakuwa vipana na kimo kikubwa.
Unaweza kujenga banda
kubwa la kawaida kwa kutumia miti inayopatikana kwenye eneo lako, mabanzi au
mbao, ambazo pia zinapatikana.
Ikiwezekana, unaweza
kujenga ukuta wa matofali na kuacha madirisha na kuziba kwa nyavu nene pamoja
na nyavu ndogo (kama za mbu) ili kuzuia wadudu wasiingie. Kumbuka kwamba,
sungura wanahitaji kupata hewa ya kutosha, lakini pia wanapenda sehemu zenye
kiza kidogo. Banda hilo lazima liezekwe vizuri ili lisivuje hasa nyakati za
masika.
Ukubwa wa banda ambalo
unaweza kulitumia kuweka vizimba vya sungura linategemea na idadi ya sungura
unaotaka kuwafuga. Wale wa kuanzia hawana shida, lakini nazungumza kuhusu
malengo ya mradi wako.
Unaweza kujenga banda
lenye upana wa futi 16 na urefu wa futi 24. Kimo cha paa la katikati ni lazima
kiwe futi 12 kuanzia kwenye sakafu na pembeni ni lazima liwe na kimo cha futi
8.
Gharama za ujenzi wa
banda la aina hiyo zitategemea na rasilimali ulizotumia kujengea.
Kama unafuga kibiashara,
weka sakafu nzuri kwa sababu utatumia njia bora za kukinga mkojo ambao ni mali.
Lakini kama hutaki kukinga mkojo, basi usisakafie ili mkojo ukidondoka uweze
kuzama ardhini na inakusaidia katika kusafisha na kuondoa harufu. Sakafu imara
ya kawaida inakupasa usafishe kila wakati, hasa kama hukutumia njia bora za
kukinga mkojo.
Lakini nakushauri, kinga
mkojo kwa sababu ni mali. Utapata fedha nyingi bila kutegemea.
Vizimba ambavyo vimeinuliwa na kutengeneza bati maalumu kwa ajili ya kukikanga mkojo.
Kama hutaki kutumia
vizimba, kamwe usiwaweke sungura wako kwenye sakafu ya udongo, kwa sababu
sungura wana kawaida ya kuchimba na unaweza kukuta wametoboa ardhi na kutoka
nje.
Sakafu ya udongo
itakufanya upate shida pia wakati sungura wanapozaa, kwani wanaweza kuzalia
kwenye mashimo.
Hivyo basi, kama
utawafuga bila kutumia vizimba, weka sakafu na uweke matandazo sakafuni.
Vizimba
Vizimba (hutches
au cages) lazima vitengenezwe kabla ya kuwaingiza sungura wako wa kwanza. Sungura
mmoja anapaswa kuwa na nafasi ya upana wa futi mbili, urefu wa futi tatu na
kimo cha futi tatu – pamoja na eneo la kutosha la kuchezea.
Unaweza
kujenga vizimba vikubwa kuwezesha kuweka sungura wengi ambao unapanga kuwalisha
tu kwa ajili ya kuwauza kwa nyama. Kwa kadiri kizimba hicho kitakavyokuwa, ni
vyema kukiinua kutoka usawa wa ardhi ili kukusaidia kuondoa takataka unapofanya
usafi.
Eneo la kuishi – wastani wa 12 sq. ft (6 x 2) ambalo linaweza kuwa na sungura wadogo na wa maumbile ya kati wanne. Ikiwa sungura wako ni wa aina ya wale wakubwa, basi unatakiwa kuongeza ukubwa wa banda.
Eneo la kuishi
la sungura wako kwenye kizimba ni lazima lihusishe eneo la kulala, eneo la
kudondoshea kinyesi na vifaa vya chakula na maji na nafasi ya kutosha ya kuweza
kucheza. Ni vyema sungura wako wakawa na eneo la kutosha kujinyoosha katika
kila upande. Eneo la kuishi la sungura wako likiwa dogo litaathiri afya yake –
na kumsababishia matatizo ya uti wa mgongo, kupoteza nyama na utapiamlo.
Upana wa kizimba
Sungura aliye
huru lazima atajinyoosha anapokuwa amepumzika, hivyo kizimba chako kinatakiwa
kiwe kipana kuwezesha sungura alale huku akiwa amenyoosha miguu yake yote. Hii
inatoa nafasi ya kutosha kuweza kujigeuza.
Wastani wa upana
unatakiwa kuwa futi 2 (60sm) kwa sungura wadogo na wa kati na futi 3 (90sm) kwa
sungura wakubwa kama wa aina ya Flemish Giants.
Urefu wa kizimba
Kizimba
kinapaswa kuwa kirefu kidogo ili kumwezesha aruke mara tatu hadi mara nne bila
kuigonga pua yake mwisho wa kizimba. Sungura wa umbile la kati anaruka kwa
umbali wa inchi 18 (45sm) kwa kila mruko mmoja.
Kama upana wa
kizimba chako ni futi 2, urefu unapaswa kuwa futi 6 ili kufanya jumla ya futi
za eneo 12.
Kimo cha kizimba
Sungura
husimama kwa miguu yao ya nyuma ili kuangalia kama mazingira yao ni salama, na
kizimba chako lazima kiwe na urefu unaomruhusu kusimama bila kujigonga kichwani
ama masikio yake kugusa juu ya dari.
Kimo cha futi 2'
(60sm) mara nyingi kinafaa kwa sungura wa ukubwa wa kati lakini aina kubwa za
sungura zinahitaji kimo cha futi 3' (90sm).
Eeneo la kuchezea – wastani 32 sq. ft.
Kiwango cha
wastani kinachopendekezwa kwa ajili ya eneo la mazoezi ni eneo la futi 32
(mfano; futi 8'x4'). Kama ilivyo kwa eneo la kulala, sungura wako atahitaji
eneo la kusimama wima. Ingawa siyo lazima, lakini husaidia sungura wako
kuongeza urefu wakati wa kuruka.
Kama
utaunganisha vipimo hivi kwa pamoja, kizimba chako kinapaswa kuwa na eneo la futi
48 (upana futi 6 x urefu futi 8).
Lakini eneo la
kuchezea tu haitoshi, bali unatakiwa kuweka na vitu ambavyo sungura atachezea
kama vipande vya vigogo ambako anaweza kupanda na kusimama, mabati unayoweza
kuyakunja kama duara ndefu ambamo anaweza kupita kana kwamba anaingia kwenye shimo
na kutokea upande wa pili, na kadhalika.
Eneo lako
likiwa kubwa, hasa kama unawafuga kwa nje, yaani kama vizimba haviko ndani ya
banda, unaweza kutengeneza eneo la kuchezea lilio bora zaidi.