WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nchini
wafanye ukaguzi katika shule ili kubaini wanafunzi hewa kwenye mpango
wa elimu bure.
“Kila
mwezi Serikali inapeleka shule zaidi ya shilingi bilioni 18 kugharamia
elimu bure na sasa tumeanza kuona udanganyifu katika sekta ya elimu kwa
kuwa na wanafunzi hewa. Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nendeni
mkafanye ukaguzi ili mpate takwimu sahihi,“ amesisitiza.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Agosti 18, 2016) alipokutana na
watumishi na viongozi wa Manispaa ya Ilala katika Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Wakuu
wa Wilaya na Maofisa Elimu mkiona takwimu ziwachanganya, ni lazima
mtoke maofisini na kwenda katika shule zilizo kwenye mpango wa elimu
bure mkafanye uhakiki wa idadi ya wanafunzi,” alionya.
Wakati huo huo
Waziri Mkuu amesema maamuzi yanayotolewa kwenye vikao vya madiwani
lazima yawe na tija na ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha fedha
zinazokusanywa zinatumika kuboresha shunghuli za maendeleo badala ya
kujilipa posho.
“Lazima
mjipange vizuri na kupunguza changamoto zinazoikabili wilaya yenu.
Malipo yote ni lazima yawe yale yaliyoainishwa katika waraka na si
vinginevyo.Mtu wa Ilala unadai nauli ya sh. 200,000; hivi unakuwa
unatoka wapi hata mimi wa Lindi silipwi nauli hiyo,” alihoji.
Waziri
Mkuu alisema ni lazima halmashauri zote nchini zizingatie sheria za
Mamlaka ya Serikali za Mitaa na watendaji wake wajiulize kama mambo
wanayoyafanya yana tija na wanawatendea haki watu wanaowatumikia.
Alisema
Serikali inataka kuwa na watumishi wanaotambua nafasi zao na
watakaofanya kazi kwa uadilifu, uaminifu pamoja na uwajibikaji mkubwa
hivyo kila mtu ahakikishe anafanya kazi vizuri na yenye matokeo chanya.
“Kuna
watu wanaona ukuu wa idara ndiyo kila kitu, hata yule anayekimbiza
mafaili hathaminiwi, hili si jambo jema! Ninyi wote ni kitu kimoja, ni
watumishi wa Serikali, hivyo kila mmoja amthamini mwenzake,” alisema.
Waziri Mkuu alisema: “Mkurugenzi
yeyote asikubali kuwa na wakuu wa Idara wasiokuwa na ushirikiano na
watumishi wengine kwa sababu hataweza kupata mafanikio ya kiutendaji
ndani ya eneo lake,”.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, AGOSTI 18, 2016.