Shule za Kinondoni zajaza wanafunzi hewa kibao

44 
Shule za msingi 68 pamoja na shule 22 za sekondari katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, zimebainika kuwa na wanafunzi hewa 5,996. Kati ya hao, wanafunzi 3,462 ni wanafunzi wa shule za msingi na 2,534 ni wanafunzi katika shule za sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Salum Hapi, ameitaja idadi hiyo jana katika ofisi yake wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya wanafunzi hewa waliopo katika wilaya yake.
“La kwanza tumemwagiza mkurugenzi kuwavua madaraka walimu wakuu 68 wa shule za msingi ambao watanyanga’nywa vyeo vyao kwa kosa la udanganyifu wa takwimu juu ya elimu bure,” alisema. “Lakini la pili tunaandikia tume ya utumishi wa walimu kupitia kwa mkurugenzi ambaye ndiyo muajiri wao kuhakikisha kwamba hatua nyingine kali za kisheria zinachukuliwa dhidi ya hawa walimu wakuu 68 wa wilaya ya Kinondoni, ambao wamedanganya katika taarifa zao na kuweka idadi ya wanafunzi hewa katika orodha ya wanafunzi wa elimu bure.”
Pia kwa upande wa walimu wakuu wa shule za Sekondari alisema, ” Walimu wakuu wa shule za sekondari wako chini ya katibu tawala wa mkoa, tumemuandikia katibu tawala wa mkoa kumuomba awavue vyeo vyao walimu wakuu 22 wa shule za sekondari zilizopo Kinondoni, ambapo wameleta takwimu za uongo na wameweka majina hewa ambapo zaidi ya milioni 60 zimekwisha kwenda kinyume na takwimu halisi katika shule zao.
Alielezea pia hatua zitakazochukuliwa dhidi wakuu hao, “Kwanza anashushwa cheo atakuwa mwalimu wa kawaida , lakini la pili atachukuliwa atachukulia hatua nyinginezo za kisheria kwa mujibu wa mamlaka ya utumishi wa walimu kwa shule za msingi na tatu atalipa fedha zote ambazo zimepelekwa kule kinyume na utaratibu kwa kutokana na udanganyifu alioufanya.”
“Hatutakuwa na huruma na mwalimu mkuu yeyote atakayefanya udanganyifu wa takwimu za elimu bure, tutamchukulia hatua kali za kisheria mwalimu yeyote ambaye ataghushi idadi ya takwimu za elimu bure kinyume na idadi halisi ya wanafunzi wa elimu bure.”
BY:EMMY MWAIPOPO

Artikel Terkait